Monday, February 17, 2014


NIMSHUKURU sana Mungu, muumba wa mbingu na ardhi kwa kuweza kutufikisha tena leo, kama alivyofanya jana, juzi na kila siku bila ya sisi kutumia gharama yoyote. Vitendo vyake kwetu ni vya utukufu mkuu, ingawa mara nyingi binadamu tumekuwa tukifanya vitu vingi vya kumkwaza.
Jaji Joseph Sinde Warioba.
Baada ya kusema maneno hayo, naomba sasa niende kwenye hoja yangu ya leo, ambayo kwa hakika ni ya msingi sana kama bado tunataka kujenga taifa lenye mshikamano, uimara na lisilo na mgawanyiko, kwa misingi ya kabila, dini wala rangi.
Wote tunajua kwamba leo, Bunge maalum la Katiba linaanza vikao vyake mjini Dodoma, likiwa na lengo moja tu, kupata katiba bora kabisa ambayo nchi yetu itaifuata kwa ajili ya ustawi wake na wananchi.
Hii ni baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Marekebisho ya Katiba, iliyoratibu maoni ya wananchi nchi nzima, iliyofanya kazi chini ya Uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake, Jaji Augustino Ramadhan.
Ingawa kumekuwa na kutokuelewana kwa hapa na pale miongoni mwa wanasiasa kuhusiana na mchakato huo, ni jambo la kushukuru kwamba hadi sasa, tunapoelekea bungeni, tumeweza kuvumiliana na kukubaliana juu ya mambo ya msingi kwenye katiba yetu.
Hata hivyo, wakati tukielekea katika hatua hii kubwa na muhimu zaidi, zipo dalili zinazoonyesha kwamba kutakuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe juu ya mambo mbalimbali. Kinachotia shaka, ni baadhi ya vitu ambavyo havionyeshi kama wajumbe hao wako makini na ustawi wa nchi yetu au la.
Ni kwa kutambua umuhimu wa kuiweka mbele nchi yetu kabla ya kitu chochote, ningependa kuwashauri wajumbe wetu kutumia zaidi busara katika mijadala yao ili historia iweze kuandikwa, vinginevyo, tunaweza kujikuta tukizalisha katiba ambayo italeta janga kwa taifa badala ya heri kama ilivyo matarajio ya kila mmoja.
Endapo kila mmoja atalazimisha kupita kwa hoja au mawazo yake, basi ni bora tukasitisha mchakato huu, ili tuufanye kwa utaratibu mwingine bora zaidi, mradi tu mwisho wa siku, iwe ni Tanzania ndiyo iliyofaidika na katiba hiyo, badala ya vyama vya siasa au asasi za kiraia zenye wajumbe wake katika bunge hilo.
Ni lazima tuelewe kuwa siyo kila hoja ya kila mjumbe itapitishwa, zipo zitakazoachwa au kuboreshwa. Wajumbe wetu lazima watazame zaidi faida ya hoja kwa taifa badala ya vyama vyao vya siasa au taasisi wanazoziwakilisha.
Kinachoonekana ni kuwa baadhi ya wajumbe hao, kwa kutotambua kwamba umuhimu wa taifa letu kuwekwa mbele, wamekwenda Dodoma wakiwa na katiba yao, kwamba ni kile tu wanachotaka wao ndicho kinachotakiwa kuwemo ndani yake.
Hii siyo sawa. Kama italazimu, ni bora kama watakubaliana katika kutokukubaliana na zoezi hilo likaahirishwa hadi wakati mwingine, mradi tu, lengo linafikiwa. Itakuwa ni kuwasaliti wananchi, kama wajumbe wetu watakubali kulazimisha kupitisha jambo ambalo wanajua wazi kabisa, halina masilahi kwa wananchi na taifa kwa ujumla wake.
Katiba ni jambo nyeti, tusilipeleke ili mradi tu tumefanya, isipokuwa tulifanye kwa weledi na mapenzi makubwa kwa nchi yetu, kwa sababu tunajua kwamba suala hili linatuhusu sisi tuliopo hivi sasa na vizazi vyetu vijavyo. Tusije kutenda jambo ambalo watoto na wajukuu zetu wakaja kutulaumu hapo baadaye.
Tanzania ni bora zaidi kuliko chama chochote cha siasa, kwa sababu tunaweza kupoteza chama chochote tukaunda kingine, lakini tukiipoteza Tanzania, kamwe hatutaweza tena kuipata popote.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

0 comments:

Post a Comment