Tuesday, March 4, 2014


Stori: Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKATI msuguano  wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ukiendelea mjini Dodoma na kuzua majadiliano makali juu ya upigaji kura ya wazi au ya siri, ngoma inogile kwani inatabiriwa kuwa huenda bunge hilo lisifikishe  siku 90 za uhai wake na kuishia siku 70, baadhi wa wajumbe wameliambia Risasi Mchanganyiko.
Wakizungumza bila ya kutaka kutajwa majina yao, baadhi ya wajumbe wa bunge hilo wamesema kuwa hali siyo shwari kutokana na baadhi ya wanasiasa kutetea misimamo yao ili ishinde.
“Tunaonekana si wamoja ndani ya bunge hili na kila upande umekuja na dhamira yake ya kutafuta ushindi, hali hii inaweza kulifanya bunge kushindwa kumaliza siku 90 zilizopangwa kutafuta Katiba Mpya ya Tanzania,” alisema mjumbe mmoja kutoka Zanzibar kwa niaba ya wenzake.
Pia wanasiasa wanaotoka katika vyama vya upinzani wamekuwa wakikishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutaka kuuteka mkutano huo.
“Asilimia kubwa ya wapinzani wanataka kura za  siri lakini CCM wanataka wajumbe wapige kura za wazi kwa maslahi yao ili kuweza kuwaadhibu wanachama wao wasiokubaliana na hoja za upande wao, kwa mtazamo huu hatutafika siku 90,” aliongeza mjumbe mwingine wa upinzani.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe  wa CCM wamewashutumu wenzao wa upinzani  kwa kuwaambia kuwa wana malengo  ya  kuvunja muungano wa Tanzania kwa ajili ya uroho wa madaraka.
“Haiwezekani tuje Dodoma kama Watanzania na tutoke  tukiwa si Watanzania, lengo letu ni kudumisha umoja na kuendeleza mazuri ya viongozi wetu waliotangulia,” alisema mbunge wa CCM anayetokea Mwanza.
Naye mwenyekiti wa  muda wa bunge hilo, Pandu Amir Kificho amekuwa katika wakati mgumu kwa kuwataka wajumbe kuacha  kuchangia rasimu ya katiba kabla ya muda wake.
“Naomba nieleweke, bado hatujaingia kuichambua rasimu ya katiba, hebu tujadili kanuni za kutuongoza kwanza,” alikaririwa mwenyekiti huyo akimwambia Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama Cha Wananchi (CUF) na kuwafanya wajumbe wengine kumshangilia.
Baadhi ya wadau wanaofuatilia bunge hilo wamesema hawatashangaa kuona wajumbe wakiondoka Dodoma kabla ya kutimia kwa siku 90.
“Hilo liko wazi, fedha za walipa kodi zinaweza kuliwa bure na Watanzania wasipate kile wanachotarajia,” alisema Othman Zinga anayefuatilia mkutano huo.

0 comments:

Post a Comment